Makonde
Kamusi hii imeandikwa katika lugha tatu. Sehemu ya kwanza inaorodhesha maneno ya Kimakonde na kuyatolea fasili za Kiingereza na Kiswahili. Sehemu ya pili inaorodhesha maneno ya Kiswahili na kuyatolea fasili kwa Kimakonde. Sehemu ya tatu inaorodhesha maneno ya Kiingereza na fasili zake kwa Kimakonde.

Mpangilio

Kamusi hii imepangwa katika utaratibu wa kawaida wenye kuonyesha maana ya kila kidahizo kwa Kiingereza na Kiswahili.Maneno yenye tahijia moja lakini maana tofauti, yaani homonimu, yameingizwa yakifuatiwa na tarakimu ndogo 1, 2, na kuendelea. Utaratibu huu umefuatwa hata kama maneno husika yanatofautishwa na toni katika matamshi. Vitenzi vimeorodheshwa kwa mzizi; lakini nomino zimeorodheshwa kwa kiambishi cha ngeli ya nomino katika umoja. Maneno mengine yenye kuchukua kiambishi cha upatanisho (hususani vivumishi, viwakilishi) yameorodheshwa kwa mzizi na alama ya “–“ kabla yake.
Mfano: -joko dogo; -kulu kubwa; -lehu refu; -vihi bichi.
Mara baada ya kidahizo kiashirio cha matamshi kinafuata – hasa kikionyesha toni za neno husika. Iwapo neno hilo ni kitenzi, matamshi yataingiza pia kiambishi ku- ambacho ni sawa na ku- katika Kiswahili.