Mpangilio

Msamiati huu una sehemu mbili. Sehemu ya kwanza inaorodhesha maneno ya Runyambo na maelezo yake katika Kiswahili na Kiingereza. Sehemu ya pili inaorodhesha maneno ya Kiingereza na maelezo yake katika Kinyambo na Kiswahili.
 
Viambishiawali katika sehemu zote mbili vimepangwa kabla ya safu ya maneno ya Runyambo, navyo ni vya aina mbili. Aina ya kwanza ni kiambishiawali cha kitenzi ku/kw. Aina ya pili ni kisabiki kiambishiawali cha nomino a/e/o, kama vile katika a-máte, e-citi, o-rúku. Karibu nomino zote zina kiambishi hiki isipokuwa nomino nyingi za ngeli ya ri (kama vile ikúru, itáma, íju …), majina ya rangi, nomino pekee (k.m Kakúru), na baadhi ya majina ya wanyama.
 
Vivumishi na viwakilishi (vionyeshi, vimilikishi, viulizi) (katika Sehemu ya Kwanza) vimewekewa alama hii(@) katika safu ya viambishi, ikiashiria kuwa vinachukua maumbo ya upatanisho kutoka kwenye nomino husika. Mbali na maumbo haya, ni maumbo machache sana yasiyochukua kisabiki kiambishiawali k.m. bâmbe, nkána, íngaaha, ánga.
 
Nomino zimeorodheshwa kialfabeti kwa kufuata kiambishi cha ngeli katika umoja. Umbo la wingi wa nomino limeingizwa iwapo
i) ndilo umbo la kawaida lililopo, kama vile a-máte, e-bica, a-magara,
ii) ndilo umbo linalojitokeza mara nyingi zaidi, k.m. iyengo/amayengo
iii) linaleta maana maalumu, k.m. e-bihinzi/e-cihinzi, e-bireju/e-cireju, ikúru/a-makúru.